MWONGOZO WA UTOAJI MIKOPO KWA WANAFUNZI WA STASHAHADA KWA MWAKA WA MASOMO 2023/2024

1.0    MAELEKEZO MUHIMU KWA WANAFUNZI WOTE WANAOOMBA MIKOPO

Waombaji wote wa mikopo ya elimu kwa ngazi ya Stashahada kwa mwaka wa masomo 2023/2024 wanafahamishwa kuzingatia mambo yafuatayo:-

  • Kusoma na kufuata taratibu za maombi katika Mwongozo wa mwaka wa masomo 2023/2024;
  • Kuhakikisha kuwa namba ya mtihani wa kidato cha nne atakayoitumia mwombaji iwe sawa na atakayoombea udahili wa chuo;
  • Kuhakikisha kuwa nyaraka zote za maombi ya mkopo anazowasilisha mwombaji ziwe zimehakikiwa na mamlaka husika;
  • Waombaji wajaze fomu zao kwa ukamilifu na kuzisaini kabla ya kuziwasilisha HESLB kwa njia ya mtandao;
  • Kuhakikisha kwamba vyeti vya kuzaliwa/vifo vimethibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) au Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA) au Afisa aliyeteuliwa ili kuthibitisha uhalali wa nyaraka hizo;
  • Kwa mwombaji mwenye taarifa zake za benki ajaze kwa usahihi kwenye fomu ya maombi ya mkopo;
  • Kwa mwombaji mwenye Namba ya simu na kitambulisho cha taifa (NIDA) ahakikishe anajaza namba hizo wakati wa kuomba mkopo.
  • Waombaji wote wanakumbushwa kuzingatia muda wa mwisho wa kutuma maombi kwa njia ya mtandao.

2.0    KUFUNGULIWA DIRISHA LA MAOMBI

Kwa wanafunzi wanaotarajia kuomba mikopo ya elimu kwa ngazi ya Stashahada, dirisha la maombi ya mkopo kwa mwaka wa masomo 2023/2024 litafunguliwa kuanzia tarehe 07 Oktoba, 2023 hadi tarehe 19 Oktoba, 2023.

SIFA STAHIKI

Sheria na Kanuni za Bodi ya Mikopo zinaainisha sifa na vigezo vya jumla kwa wanafunzi wanaohitaji mkopo baada ya kudahiliwa na vyuo vyenye ithibati. Mwombaji atatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-

3.1       Vigezo vya Msingi vya Mwombaji Mkopo

  • Awe Mtanzania mwenye umri usiozidi miaka 27 wakati wa kuomba mkopo;
  • Awe amedahiliwa katika taasisi ya elimu inayotoa elimu ya ngazi ya kati nchini;
  • Awe amekamilisha na kuwasilisha maombi ya mkopo kupitia mfumo wa maombi ya mkopo (OLAMS);
  • Asiwe na ajira au mkataba wa kazi wa serikalini au sekta binafsi unaompatia mshahara au kipato;
  • Awe amehitimu elimu ya kidato cha nne (CSEE), Cheti (astashahada) au kidato cha sita (ACSEE) au ndani ya miaka mitano; yaani kati ya mwaka 2019 hadi 2023.

3.2    Hali ya Kijamii na Kiuchumi

  • Uyatima; aliyefiwa na mzazi au wazazi
  • Familia au kaya ya kipato duni inayofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) au taasisi nyingine za kitaifa zinazotoa ufadhili kwa kaya zenye vipato duni;
  • Ulemavu wa mwombaji au wazazi wake.

4.0    UPANGAJI WA MIKOPO

Upangaji wa mikopo utazingatia vipaumbele vifuatavyo:-

  • Mwanafunzi mwenye udahili kwenye programu za vipaumbele vya Taifa kama zilivyofafanuliwa katika Kipengele cha 6 cha Mwongozo huu zitazingatiwa;
  • Ufaulu wa kitaaluma uliomuwezesha kudahiliwa kwa ajili ya elimu ya ngazi ya kati; na
  • Hali ya kijamii kama ilivyofafanuliwa katika kipengele cha 3.2 cha mwongozo huu.

5.0    NYARAKA ZA KUAMBATISHA WAKATI WA MAOMBI YA MKOPO

Zifuatazo ni nyaraka muhimu za kuambatisha kwenye maombi ya mkopo: –

  • Cheti cha kuzaliwa kutoka mamlaka husika, ZCSRA kwa waombaji kutoka Zanzibar au namba ya uhakiki (verification number) kutoka RITA kwa waombaji kutoka Tanzania Bara;
  • Vyeti vya vifo vya wazazi kuthibitisha uyatima kutoka mamlaka husika, ZCSRA kwa waombaji kutoka Zanzibar au namba ya uhakiki (verification number) kutoka RITA kwa waombaji kutoka Tanzania Bara;
  • Fomu ya kuthibitisha Ulemavu wa mwombaji iliyoidhinishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) au Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO);
  • Fomu ya kuthibitisha Ulemavu wa mzazi wa mwombaji iliyoidhinishwa na Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) au Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO);
  • Namba ya kaya ya Mnufaika kutoka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

6.0    MAENEO NA PROGRAMU ZA KIPAUMBELE KATIKA UTOAJI WA MIKOPO

6.1    Maeneo ya Kipaumbele

Mkopo utatolewa katika maeneo makuu sita yakiakisi vipaumbele vya Taifa kama ilivyoainishwa katika tangazo la Serikali Namba 715 la tarehe 29 Septemba 2023. Maeneo hayo ni kama ifuatavyo:-

  • Afya na Sayansi Shirikishi (‘Health & Allied Sciences’);
  • Elimu ya Ualimu (‘Education and Teaching’);
  • Usafiri na Usafirishaji (‘Transport & Logistics’);
  • Uhandisi wa nishati (‘Energy Engineering’);
  • Madini na Sayansi ya ardhi (‘Mining & Earth Science’) na
  • Kilimo na Mifugo (‘Agriculture & livestock’)

6.2    Programu za kipaumbele

Katika mwaka wa masomo 2023/2024 mikopo itatolewa kwa wanafunzi waliodahiliwa katika Program/Stashahada zinazoangukia/zilizomo katika maeneo sita ya kipaumbele yaliyoidhinishwa – rejea kipengele 6.

6.2.1      Afya na Sayansi Shirikishi (Health & Allied Sciences)

Programu katika kundi hili ni kama zifuatazo:-

  • ‘Clinical Dentistry’;
  • ‘Diagnostic Radiotherapy’;
  • ‘Occupational Therapy’;
  • ‘Physiotherapy’;
  • ‘Clinical optometry’;
  • ‘Dental Laboratory technology’;
  • ‘Orthotics & Prosthetics’;
  • ‘Health record & information’;na
  • ‘Electrical and Biomedical Engineering’.

6.2.2      Elimu ya Ualimu (Education and Teaching)

Programu katika kundi hili ni kama zifutazo:-

  • Stashahada za msingi za Ualimu: Stashahada ya Ualimu wa Sayansi katika masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati; na
  • Stashahada za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TE&VET).

6.2.3  Usafiri na usafirishaji (‘Transport and Logistics’)

Programu katika kundi hili ni kama zifuatazo:-

  • ‘Aircraft Mechanics’;
  • ‘Ship building and repair’;
  • ‘Railway construction and maintenance’; na
  • ‘Global Logistics and Supply Chain Management.

6.2.4      Uhandisi wa nishati (‘Energy Engineering’)

Programu katika kundi hili ni kama zifuatazo:-

  • ‘Renewable Energy Engineering (Hydro, Wind, Solar)’; na
  • ‘Pipeline, Oil and Gas Engineering’.

6.2.5      Madini na sayansi ya sayari (‘Mining and Earth Science’)

Programu katika kundi hili ni kama zifuatazo:-

  • ‘Lapidary and Jewelry’; na
  • ‘Mineral Processing’.

6.2.6      Kilimo na Ufugaji (‘Agriculture and Livestock’)

Programu katika kundi hili ni kama zifuatazo:-

  • ‘Leather Technology’;
  • ‘Food Technology and Human Nutrition’;
  • ‘Sugar Production Technology’;
  • ‘Veterinary Laboratory Technology’;
  • ‘Horticulture’;
  • ‘Irrigation Engineering’; na
  • ‘Agro Mechanization’.

7.0    VIPENGELE NA VIWANGO VYA MKOPO

Waombaji watakaopangiwa mikopo watapangiwa viwango vya fedha kulingana na mahitaji halisi ya vyuoni. Mkopo utagawanywa katika vipengele vya mkopo kwa mtiririko ufuatao: Chakula na Malazi, Ada ya Mafunzo, Gharama za Vitabu na viandikwa, Mahitaji maalumu ya Kitivo, Gharama za Utafiti na Mafunzo kwa Vitendo.

Mkopo utatolewa kwaajili ya kugharamia vipengele vyote au baadhi ya vipengele, kama itakavyochambuliwa na kuidhinishwa.

7.1         Chakula na Malazi

Kiwango cha juu kisichozidi TZS. 7,500.00 kwa siku kitatolewa kulingana na idadi ya siku mwanafunzi atakazokuwa chuoni kama inavyoelekezwa kwenye kalenda ya chuo husika. Kiasi hiki kitalipwa moja kwa moja kwa mwanafunzi.

7.2         Ada ya Mafunzo

Kiwango cha juu cha ada kisichozidi TZS. 1,400,000.00 kwa mwaka kulingana na gharama zinazolipwa katika chuo husika kwa mwaka na kitalipwa moja kwa moja kwa chuo husika.

7.3         Gharama za Vitabu na Viandikwa

Kiwango cha juu cha kisichozidi TZS. 200,000.00 kwa mwaka kwa vitabu na viandikwa na kitatolewa kwa wanafunzi.

7.4         Mahitaji Maalumu ya Kitivo

Kiwango cha juu kisichozidi TZS. 300,000.00 kwa mwaka kulingana na gharama husika zitalipwa moja kwa moja chuoni.

7.5         Mafunzo kwa Vitendo

Kiwango cha juu kisichozidi TZS. 7,500.00 kwa siku hadi siku 56 kwa mwaka, kwa ajili ya Mafunzo kwa Vitendo kitatolewa. Kiasi hicho kitalipwa moja kwa moja kwa mwanafunzi.

7.6    Gharama za Utafiti

Kiasi kisichozidi TZS. 100,000.00 kwa mwaka kitatolewa kwa gharama za utafiti (Project) kwa baadhi ya program kama zilivyoainishwa na chuo husika.

8.0    MASHARTI MENGINE

8.1    Wajibu wa Mdhamini na Mzazi/Mlezi

Wazazi/Walezi na wadhamini wana wajibu wa kuthibitisha usahihi wa taarifa ambazo zitawasilishwa katika fomu ya maombi ya mkopo kabla ya kusaini. Mdhamini/Mzazi atatakiwa kuhakikisha kwamba mkopaji anajaza taarifa sahihi zitakazotumika wakati wa urejeshaji. Aidha mdhamini atatakiwa kutoa taarifa za mkopaji na makazi pale atakapochelewa au kushindwa kurejesha mkopo wake.

Kwa mwanafunzi alie na umri chini ya miaka 18 wakati wa kuomba mkopo atalazimika kujaza tamko rasmi (declaration) kuridhia kuendelea kupokea mkopo pindi atakapotimiza umri wa miaka 18.

Mwombaji wa mkopo anapaswa kuambatanisha picha (passport size) ya mdhamini na nakala ya kitambulisho kimojawapo kati ya vilivyotajwa hapo chini ambacho kimetolewa na mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Serikali ya Mapinduzi Zanzibar:-

  • Kitambulisho cha Taifa
  • Kadi ya mpiga kura
  • Leseni ya udereva
  • Pasi ya kusafiria
  • Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi

8.2    Urejeshaji Mkopo

Baada ya kuhitimu masomo ya elimu ya kati, mnufaika wa mkopo atatakiwa kurejesha mkopo wake wote kwa makato yasiyopungua asilimia kumi na tano (15%) ya mshahara wake wa kila mwezi au kiwango kisichopungua TZS 100,000.00 kwa mwezi kwa Mnufaika aliyejiajiri kwenye sekta isiyo rasmi. Iwapo mnufaika ataachishwa/atakatisha masomo, mkopo huo wote utalipwa kwa mkupuo. Mikopo yote inatozwa asilimia moja (1%) ya ada ya uendeshaji kwenye deni la msingi la mnufaika kwa mara moja.

9.0    KUHAMA CHUO AU PROGRAMU NDANI YA CHUO

Endapo Mnufaika wa mkopo atabadilisha programu ya masomo ndani ya chuo chake, mkopo/stahili zake zitahamishwa na HESLB baada ya kupokea uthibitisho wa chuo chake. HESLB haitafanya malipo kwa wanafunzi ambao watahamia vyuo vingine kwa hiari yao ama kuhamia programu ambazo sio za kipaumbele zilizotajwa katika kipengele cha 6 cha mwongozo huu.

Uhamisho wa mkopo hautabadilisha kiwango cha mkopo kilichopangwa awali isipokuwa tu pale ambapo mwanafunzi amehamishwa na mamlaka.

10.0 JINSI YA KUOMBA

Maombi yote ya mkopo yatafanyika kupitia Mfumo wa Maombi na Usimamizi wa Mikopo (OLAMS). Waombaji wote wa mikopo WANAKUMBUSHWA kutumia namba ileile ya Mtihani wa Kidato cha Nne iliyotumika wakati wa udahili.

Baada ya kukamilika kwa mchakato wa maombi kwenye mtandao, waombaji watapaswa kupakua nakala za fomu za maombi na mikataba ya mkopo kwenye mtandao, kugonga mihuri sehemu husika, kusaini fomu, kuambatanisha nyaraka zinazohitajika na kuziwasilisha kurasa zilizosainiwa (namba 2 na 5) ya fomu ya maombi katika OLAMS.

Mwombaji anatakiwa kupakua fomu sahihi kwa kuzingatia fomu ya mwombaji aliye na umri chini ya miaka 18 ama aliye juu ya miaka 18.

11.0 ADA YA MAOMBI YA MKOPO

Waombaji wanapaswa kulipia ada ya maombi ya mkopo ya kiasi cha shilingi elfu thelathini (30,000.00) kwa namba ya kumbukumbu ya malipo wanayoipata katika mfumo na kulipia kupitia Benki (NMB, CRDB, TCB, NBC) au kwa mitandao ya simu

(Airtel  Money,  HaloPesa,  T-Pesa,  AzamPesa,  M-Pesa,  EzyPesa/TigoPesa).

Kwa maelezo zaidi tembelea: https://olas.heslb.go.tz.

12.0 ORODHA YA WAOMBAJI WATAKAOPANGIWA MIKOPO

Orodha ya waombaji mikopo watakaopangiwa mikopo itatangazwa kupitia akaunti za kudumu za waombaji mikopo (SIPA) zilizotumiwa wakati wa kuomba mkopo au kwenye tovuti ya HESLB: www.heslb.go.tz baada ya mikopo kuidhinishwa.

13.0 MAULIZO NA MALALAMIKO

Waombaji au wanufaika wa mikopo wenye maswali au malalamiko watapaswa kufuata taratibu zilizoainishwa kwenye dawati la msaada la dirisha la maombi ya mkopo.

Imetolewa na:-

MKURUGENZI MTENDAJI

OKTOBA, 2023

Pin It on Pinterest